Thursday 20 September 2012

BAVICHA WALIA NA KIKWETE

BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo, BAVICHA, limemtaka Rais Jakaya Kikwete na serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuiepusha nchi katika machafuko kwa kuwawajibisha haraka viongozi wa dola katika Wizara ya Mambo ya Ndani kutokana na tuhuma za unyanyasaji, mateso na mauaji kwa raia wasio na hatia endapo wao hawataki kujitoa.

Waliotajwa wajiuzulu au wawajibishwe na Rais kwa maslahi ya umma ni Waziri wa Mambo ya Ndani Dk. Emanuel Nchimbi na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Saidi Mwema.

Aidha Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Paul Chagonja, kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Faustin Shilogile, Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, na wakuu wa kikosi cha kutuliza ghasia mikoa hiyo wamependekeza washtakiwe.

Akisoma maazimio ya baraza hilo la taifa lililofanyika mjini hapa kwa siku tatu, Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, John Heche, alisema tayari serikali imeiweka nchi rehani kutokana na kufumbia macho matukio hayo yanayoendelea kufanywa na vyombo vya usalama.

“Mpaka sasa wananchi hawana imani na serikali yao hususan Jeshi la Polisi na haya matukio yameubadilisha ulimwengu jinsi polisi wanavyoendesha unyama kwa raia wasio na hatia kwa visingizio visivyo na maana,” alisema Heche.

Akifafanua juu maazimio 10 yaliyofikiwa na ya baraza hilo, Heche alisema kwa muda mrefu Jeshi la Polisi limekuwa likitumika kama kivuli cha Chama cha Mapinduzi kuficha uovu wake na lenyewe kujificha kwa chama hicho.

“Uone nchi hii inavyokwenda, huyu Kamuhanda aliua watu wanne Songea kumlinda kahamishiwa Iringa nako amefanya hayo hayo mpaka sasa hajakamatwa, huyo Shilogile aliua hapa Morogoro anafunikwafunikwa na hawa wote wamekuwa wakilindwa na makao makuu kupitia mkuu wa operesheni jeshi la polisi Paul Chagonja ambaye anaeneza uongo kwa umma kuwalinda polisi wenzie,” aliongeza.

Katika maazimio hayo likiwemo la kuwataka kujiuzulu, kuwajibishwa au kufunguliwa kosa la mauaji kwa mantiki ya ‘Common intention’ viongozi hao, BAVICHA pia lilimtaka Rais Kikwete kuunda tume huru ya kiuchunguzi ya kimahakama katika makosa yote yaliyotokea Arusha, Arumeru, Igunga, Ndago-Singida, Morogoro na Iringa.

Aidha baraza hilo linakusudia kuunda kikosi kitakachotafiti matatizo ya vijana likiwemo suala la elimu duni na ukosefu wa ajira na kutoa ushauri juu ya mustakabli wa taifa baada ya 2015, kuendelea kuwaunga mkono walalahoi nchini wakiwemo machinga, na imelaani CCM kuwatumia vijana katika mafunzo ya kijasusi kwani yanalenga kulichafua taifa.

Mbali na maazimio hayo pia baraza hili limetoa tahadhari kwa vyombo vya dola na Msajili wa Vyama vya Siasa John Tendwa kuepusha kauli za vitisho zinazohatarisha amani ya nchi huku wakimshauri kuifuta CCM kwa kufundisha ujasusi.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA Sharifa Suleiman alisema baraza limepitia na kuchambua kwa kina mustakabali wa kisiasa, vijana na sintofahamu iliyopo na inayozidi kudhihirika kuwa uongozi uliopo umeshindwa kuongoza hasa katika kusimamia rasilimali za nchi kwa faida ya Watanzania.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment

Chadema UK Ndani ya Milton Keynes

DAR NI SISI - VIDEO MAISHA YA WANADAR HATA BAADA YA MIAKA50 YA UHURU