Monday 17 September 2012

Mbunge: Mwenge wa uhuru marufuku , Adai ukifika jimboni kwake ataongoza kuuzima

MBUNGE wa Arumeru Mashariki, mkoani Arusha, kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Joshua Nassari, ameshikilia msimamo wa kupiga marufuku Mwenge wa Uhuru kufika jimboni kwake na kuwataka wananchi kuupuuza akidai hauna tija kwa maendeleo yao.

Aliwataka wananchi jimboni humo wakae mkao wa kula kwani jitihada za kuyatwaa mashamba makubwa yanayomilikiwa na wageni, zinaendelea hivyo wawe wavumilivu.

Bw. Nassari aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika mkutano wa hadhara wa Operesheni Sangara uliofanyika kwenye Kata ya Usa River, wilayani humo.

Aliwaataka wananchi kuupuuza mwenge huo, kutoshiriki kuchangia mchango wowote na kusisitiza kama mtu yeyote atabughudhiwa kutokana na ujio wa mwenge amualifu.

“Sioni sababu ya Mwenge wa Uhuru kukimbizwa maeneo mbalimbali nchini kwani badala ya kuhamasisha maendeleo, umegeuka sehemu ya ufujaji wa fedha za wananchi.

“Hali hii inachangia umaskini wa Taifa na kuhamasiha maovu katika maeneo yote ambayo mwengu huu unalala, nasema hivi, Mwenge wa Uhuru marufuku kufika jimboni kwangu.

“Mtu yeyote ambaye ataombwa mchango kwa ajili ya mwenge muiteni mwizi na mimi nitakuwa wa kwanza kuuzima baada ya kufika jimboni kwangu,” alisema Bw. Nassari.

Aliwataka wananchi hao kuendelea kushiriki shughuli za maendeleo bila kujali itikadi zao kisiasa na kuihadharisha Halmashauri ya Meru kuzingatia maadili ya utendaji kazi na kuacha kuwabughudhi wananchi kwa kuwachukulia bidhaa zao hasa wanapokusanya ushuru sokoni kupitia wakala wao.

Akizungumzia suala la uvamizi wa mashamba, Bw. Nassari
aliwataka wananchi kuwa wapole kwani anaandaa mkakati wa kuhakikisha ndani ya miaka mitatu, wamiliki wa mashamba hayo wanakimbia wenyewe ili wananchi waweze kujitwalia ardhi yao.

Katika hatua nyingine, Bw. Nassari alisema fedha zilizotengwa na halmashauri kwa maendeleo Kata ya Usa River, kuanzia Julai mosi mwaka huu hadi June mwaka 2013, ni sh. milioni 54.3 ambazo zitatumika kuboresha miundombinu na huduma ya maji safi.

Alisema ukarabati wa barabara kutoka Usa River hadi Magadilishu umetengewa sh. milioni nane na barabara za mji mdogo katika kata hiyo zenye urefu wa kilometa tano, zitagharimu sh. milioni 75.

Katika mkutano huo, wafuasi 15 kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), na Tanzania Labour Party (TLP) walitangaza kuvihama vyao vyao na kujiunga CHADEMA.


Majira

No comments:

Post a Comment

Chadema UK Ndani ya Milton Keynes

DAR NI SISI - VIDEO MAISHA YA WANADAR HATA BAADA YA MIAKA50 YA UHURU