Sunday 30 September 2012

Mdee `amshukia` Mchungaji Lwakatare

Serikali imetakiwa kumdhibiti na kumuondoa, kisha kuibomoa nyumba ya Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mchungaji Getrude Lwakatare.
Rai hiyo imetolewa na Waziri Kivuli, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee.
Taarifa kwa vyombo vya habari jana ilieleza kuwa, wakati raia wengine wakibomolewa nyumba ambazo kama ilivyo ya Mchungaji Lwakatare, zilijengwa kinyume cha sheria, Mbunge huyo amehamia na kuishi kwenye nyumba yake.
Julai mwaka huu, nyumba za wananchi waliojenga katika maeneo tengefu ya ufukwe wa Jangwani, mto Ndumbwi na mto Mbezi, zilibomolewa katika operesheni iliyoendeshwa na Baraza la Mazingira la Taifa (Nemc).
Operesheni ambayo ilihusisha takriban nyumba 15 na kuta nane. Lakini nyumba ya Mchungaji Lwakatare haikuguswa.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Terezya Huvisa, aliwahi kuwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma kuwa, nyumba hiyo haikubomolewa kutokana na pingamizi la mahakama.
Nyumba inayotajwa kuwa mali ya Mchungaji Lwakatare, imejengwa kwenye viwanja namba 2019-2020 Kawe Beach, katika fukwe za bahari ya Hindi.
Viwanja hivyo vinadaiwa kupatikana kwa ushirikiano wa Mchungaji Lwakatare na Frank Mushi.
Mdee alisema wakati kigogo huyo (Lwakatare) amehamia kwenye nyumba yake kwa matangazo na mbwembwe, mto Ndumbwi, bahari na mazingira kwa ujumla yameharibiwa, lakini zaidi kuwepo raia waliobomolewa kwa mujibu wa sheria hizo.
Mdee alinukuu Sheria ya Mazingira, sura 191 ya mwaka 2004, fungu 57(1), inasema hairuhusiwi kufanya shughuli zozote za kudumu za kibinadamu ndani ya mita 60.
Mita hizi ni ambazo kwa asili yake zinaweza kuhatarisha au kuathiri ulinzi na utunzaji wa mazingira, utunzaji wa bahari, kingo za mto, bwawa au mwambao wa asili wa ziwa.
Sheria nyingine ni ya ardhi, namba 4 ya mwaka 1999, sura 113, fungu la 7 (1) (d), ikieleza kwamba eneo lolote lililo ndani ya mita 60 kutoka kingo ya mto na bahari, linatakiwa kutangazwa kama ardhi hatari au kuhifadhiwa.
Na pale inapotokea kuwa masharti ya sheria moja yanapingana na masharti ya Sheria ya Mazingira, kuhusu mambo yanayohusu usimamizi wa mazingira, sheria hiyo inatumika, kwa mujibu wa fungu 232 la sheria ya mazingira sura 191 ya mwaka 2004.
”Kutokana na hali hii, serikali inatakiwa kujinasua katika mwendelezo wa tafsiri wanayoipata wananchi kuwa imetekwa na kuwekwa mfukoni na watu wachache wenye uwezo,” alisema.
Aliongeza,” maana wanaona kuwa huu ni mwendelezo wa serikali kuwa na kigugumizi pale sheria zinapovunjwa na vigogo serikalini, au watu wenye fedha wanaoshirikiana na baadhi ya viongozi wa serikali na chama tawala kufanya ufisadi.”
Alisema hali ilivyo sahihi inadhihirika kuwepo kundi la wanaojiona wapo juu ya sheria, huku wanyonge wakishughulikiwa.
”Ni wakati kwa mawaziri wanaohusika na masuala ya ardhi na mazingira kuwaeleza Watanzania kulikoni wananchi wa hali ya chini kuvunjiwa nyumba wakati Mchungaji Lwakatare, ambaye uharibifu wake ni wa hatari kuliko waliovunjiwa akitamba mtaani, ” alidai.
Mdee alitafsiri kitendo hicho kama ni Mchungaji Lwakatare kutamba kuwa yuko juu ya sheria na hakuna mamlaka yoyote yenye uwezo wa kumzuia kufanya alichofanya.
”Ni aibu kwa Taifa kuwa na viongozi wa aina hii! Viongozi ambao wako tayari kutumia fedha, hila, mamlaka na dhamana za uongozi walizopewa, kuhalalisha haramu, ni janga kwa mstakabali wa taifa letu,” alisema.
Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Terezya Huvisa, hawakupatikana kuelezea juu ya tamko la Mdee.
Mawaziri hao walikaririwa kwa nyakati tofauti wakisema nyumba zote zilizojengwa kando kando ya fukwe za bahari na mito zitabomolewa

No comments:

Post a Comment

Chadema UK Ndani ya Milton Keynes

DAR NI SISI - VIDEO MAISHA YA WANADAR HATA BAADA YA MIAKA50 YA UHURU